MWANZONI mwa mwezi huu, taifa lilianza Maonesho ya Kilimo ya Wakulima ya Nane ane kwa kushirikisha wadau mbalimbali, wengi wao wakiwa wakulima, wavuvi na wafugaji.
Maonesho hayo hufanyika kila mwaka kikanda katika maeneo tofauti na kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika Kanda ya Kati katika mkoa wa Dodoma.
Katika maadhimisho hayo, wadau mbalimbali wanashiriki, ikiwemo taasisi za fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji, nidhamu ya matumizi ya fedha hasa zinazotokana na mikopo.
Wengine ambao hawajabaki nyuma ni wanunuzi wa bidhaa zinazooneshwa katika maonesho hayo kutoka fursa kwa washiriki kutangaza bidhaa zao na kupata soko la uhakika.
Pamoja nao wengine walioshiriki wageni raia kutoka nje, ambao hutoa fursa kwa waandaji wa bidhaa zao kupata masoko ya ndani ya nje ya Tanzania na kukuza kipato na taifa kupata mapato ikiwemo fedha za kigeni.
Maofisa ugani nao hawajabaki nyuma kwa kushiriki kikamilifu maonesho hayo kwa kutoa elimu ya ukulima bora na wa kisasa kwa kuwahimiza wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo kwa lengo la kuendesha kilimo chenye tija na kubadilisha maisha yao kwa kupata kipato.
Kuna kila sababu ya kuipogenza serikali kwa kuwezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo kwani ni fursa pekee ya kuwahimiza wakulima kuzalisha chakula kingi zaidi kwa ajili ya matumizi ya familia zao na kupata ziada zaidi na kuuzwa kwenye miji mbalimbali ambako kuna mahitaji makubwa kutokana na kutokuwa na ardhi ya inayokubali mazao kustawi.
Watanzania walio wengi hususani wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wamemsikia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaagiza maofisa ugani wa kanda hiyo kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu kwa wakulima wa maeneo wanayoyahudumia ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kudhitibi uharibifu wa mazingira.
Majaliwa anatoa agizo hilo katika hotuba yake inayosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, kwenye ufunguzi wa Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika Uwanja wa John Mwakangale Mbeya.
Kwa mujibu wa takwimu za msimu wa kilimo wa 2024/2025 mikoa hiyo ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Njombe na Songwe ilipokea zaidi ya tani 485,000 za mbolea ikiwa ni ongezeko la zaidi ya tani 150,000 ikilinganishwa na msimu wa 2023/2024 tani 315,000 pekee.
Na kwa mwaka huu serikali, imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 194 kwa ajili ya mbolea ya ruzuku kwa hiyo kwa wakulima kutekeleza takwa la serikali na si kujisahau kwa kuanza kutoa visingizio kibao.
Ni faraja kusikia kuwa katika msimu uliopita wa kilimo mikoa hiyo ambayo ni ghala la taifa la chakula kuzalisha zaidi ya tani milioni 13 ya mazao ya chakula, kati ya hizo inahitaji tani milioni tatu pekee ya chakula na kubaki na ziada ya zaidi ya tani milioni 9.9 kulisha maeneo mengine.
Pamoja na mafanikio hayo, inakabiliwa na tatizo la baadhi ya wakulima kukiuka ushauri wa maofisa ugani na kupata tija ndogo kwenye uzalishaji wa mazao.
Huku wakulima wengine wamebainika kuwa wanatumia mbolea zisizostahili kwenye maeneo yao na viuatilifu ambavyo havishauriwi kulingana na mazingira, hivo kupata hasara.
Pia kuna idadi kubwa ya wakulima wanaendelea kutumia jembe la mkono kwa kilimo, halina tija badala yake wanatakiwa kutumia teknolojia za kisasa kwenye uzalishaji, ikiwa ni pamoja na matrekta na kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha mazao kwa kipindi cha mwaka mzima.
Vilevile ni faraja kusikia kuwa Vyama vya Ushirika Tanzania, vimetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.2 kwa wanachama wake ambao ni wakulima hao wakiwemo hao wa Nyanda za Juu Kusini ili waendeshe kilimo chenye tija.
Hivyo ni vyema wakulima hao kuhakikisha juhudi za serikali na vyama hivyo hazipotei bure bali ziwe chachu ya kuendelea kuleta mapinduzi katika kilimo nchini na kulisha mataifa mengi zaidi duniani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED