TAYARI Bodi ya Ligi imeshatangaza kuwa Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu wa 2025/26 utaanza Septemba 26 mwaka huu.
Jumla ya timu 16 za Ligi Kuu zitakuwa kwenye heka heka za kuusaka Ubingwa wa Tanzania Bara, pamoja na nafasi za kucheza mechi za kimataifa.
Mpaka sasa bado Bodi ya Ligi haijatoa ratiba ya ligi hiyo. Mashabiki wa soka na hata viongozi wa klabu wanasubiri ratiba hiyo kwa hamu kila mmoja akitaka kujua ataanza na nani, baadaye atacheza na nani, ataanza nyumbani au ugenini na vitu kama hivyo.
Wakati kila timu ikisubiri ratiba, binafsi nina ushauri kwa Bodi ya Ligi kuna vitu ambavyo inatakiwa ivifanyie kazi ili kuifanya kuwa ya haki na bila kuzipendelea au kuzibeba timu nyingine.
Ni ukweli usiopingika kwa wadhamini walioingia mkataba nao wana haki ya kupanga tarehe na siku zao ambazo watapata nafasi ya kuonesha michezo yote. Wana haki ya kupanga mechi kucheza kuanzia Jumatatu hadi Jumapili, na muda wowote wanaoona unafaa.
Kama kuna viwanja ambavyo vina taa, wana haki ya kutaka ratiba iwe na michezo mitatu kwa siku, mmoja ukichezwa saa nane mchana, wa pili saa 10:00 na wa tatu usiku kwenye uwanja ambao una taa kama vile Mkwakwani, Tanga, Kaitaba, Jamhuri Dodoma na Azam Complex.
Habari njema ni kwa kuelekea msimu ujao, Uwanja wa KMC nao utakuwa na taa, hivyo utaingia kwenye orodha ya viwanja ambavyo mechi zao zitacheza usiku. Kwa maana hiyo siku moja kuna uwezo wa kushuhudiwa timu tatu zikicheza bila matatizo yoyote.
Binafsi sikubaliani na baadhi ya mashabiki na wachambuzi ambao wanadai kuwa Simba na Yanga nazo zicheze saa nane mchana. Hili kwangu naona haiwezekani.
Ni ukweli usiopingika kuwa klabu hizi zina mashabiki wengi sana nchini na wangehitaji muda wa kwenda kuziangalia uwanjani na hata kwenye televisheni.
Kuzipangia saa nane mchana wakati iwe katikati ya wiki au wikiendi ni kuwakosea heshima mashabiki wao ambao muda huo wanakuwa kazini, wikiendi wengine wanakuwa kwenye ibada, baadhi ni siku ya kuangalia wagonjwa na kusalimia ndugu, hivyo sioni kama kuna haja sana ya kuzipangia mchana.
Ikumbukwe kuwa Simba na Yanga ndizo timu zinazokusanya mashabiki wengi viwanjani kuliko mechi zingine hivyo ni lazima kuziangalia na jicho lingine. Hata timu nyingine za mikoani zisingependa Simba na Yanga ziende kucheza mechi zao mapema, kwani watakosa mapato.
Ikumbukwe timu za mikoani huchukua mapato yote, Simba na Yanga zinapokwenda kucheza huko, licha ya kwanza asilimia kuwa ya mashabiki huwa ni wa timu hizo kongwe. Nazo pia zisingependa kuona mechi za Simba na Yanga zikicheza saa nane.
Ninachoshauri kwa bodi ni kuziangalia timu zinaitwa au kujiita ndogo kwa jicho la huruma zisipangiwe mechi za zinazokaribiana kwenye ratiba. Utakuta timu imecheza Jumamosi Lindi dhidi ya Namungo FC, halafu inatakiwa Jumatano iende ikacheze Kigoma na Mashujaa FC.
Kutoka Lindi mpaka Kigoma kuna umbali mkubwa sana. Hali hiyo inaziumiza sana, ikizingatiwa nyingi hazitumii usafiri wa ndege kwani hazina uwezo huo, badala yake zinatumia basi. Angalau timu ikicheza Lindi, Jumamosi basi Jumatatu ikacheze Dar es Salaam na si Kigoma, Mwanza au Kagera.
Tumeshashuhudia matukio mengine ya kusikitisha, Simba au Yanga inakwenda kucheza labda na Pamba Jiji, CCM Kirumba, Mwanza, zenyewe zinakwenda na ndege na kufika mapema. Lakini mwenyeji wakati huo anakuwa ametoka kucheza Mbeya na Prisons.
Hana nauli ya ndege. Timu inatembea kwa umbali mrefu hadi kufika nyumbani Mwanza na kuwakuta wageni wao wameshakuwa wenyeji. Uchovu unawafanya kupoteza mechi na si ufundi. Hili nalo bodi iliangalie.
Angalau timu zinazocheza na Simba, Yanga au Azam zinapokwenda ugenini ziwakute wenyeji wamecheza mechi hapo hapo nyumbani, au mikoa jirani. Hii itazisaidia sana timu ambazo hazina uwezo wa kusafiri kwa ndege.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED