UTAFITI mpya wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto na vijana mwaka 2024 uliotolewa hivi karibuni, unaonesha ukatili wa kingono, kihisia na kimwili kwa watoto umepungua ikilinganishwa na utafiti uliofanyika mwaka 2009.
Kwa mujibu wa utafiti huo mpya, ukatili wa kingono kwa watoto wa kike umepungua kutoka asilimia 33 hadi asilimia 11, kimwili ni kutoka asilimia 76 hadi asilimia 24 na kihisia kutoka asilimia 25 hadi asilimia 22.
Aidha, ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume, umepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia tano, wa kimwili umepungua kutoka asilimia 74 hadi asilimia 21 na kihisia umepungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 16.
Matokeo ya utafiti huo yalitolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima hivi karibuni kwamba ulifanyika kati ya Machi na Juni, 2024 na uliwafikia zaidi ya watoto 11,414 wenye umri wa miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Matokeo ya utafiti huu yataiwezesha serikali na wadau wake kuboresha na kuandaa mipango, programu na mikakati mbalimbali ya kutokomeza vitendo hiyo na kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na vijana kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.
Hivyo, bado ipo haja ya kutafuta ufumbuzi zaidi kwenye suala la ukatili wa kijinsia hasa uwepo wa ndoa za utotoni, ambao umekuwa ukikatisha ndoto za watoto wa kike katika elimu na pia kuhataria afya zao.
Baadhi ya vyanzo vya ndoa hizo vimekuwa vikitajwa kuwa ni umaskini wa kipato na mila na desturi zilizopitwa na wakati ambavyo husababisha watoto wa kike kuingizwa kwenye ndoa.
Umri wa kuolewa, umekuwa ni miongoni mwa mambo yanajadiliwa kwa muda mrefu na watu wa kada mbalimbali katika vyombo vya habari na mitanadao ya kijamii, huku kukiwa na maoni yanayopingana.
Wapo baadhi ya watu ambao wanataka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11 hadi 13 ambaye amevunja ungo, aruhusiwe kuolewa kwa amri ya mahakama, kwa kuzingatia vielelezo vya kimazingira ikiwamo afya.
Lakini pia wapo wengine ambao wanapendekeza Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ifanyiwe marekebisho hasa katika vifungu vya 13 na 17, kwa maelezo kuwa vinaruhusu mtoto wa miaka 15 aolewe kwa ridhaa ya wazazi.
Pamoja na hayo, ninaamini kwamba ndoa za utotoni ni tatizo, kwani zinaweza kusababisha watoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao katika elimu, hali duni za maisha na madhara ya kiafya kwa mabinti.
Ndoa za utotoni zinatajwa kama mateso, ambao wadau wa kutetea haki za binadamu, wakiwamo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wanatamani umri wa kuolewa uanzie miaka 18.
Wanazingatia Sheria ya Mtoto ya Mmwaka 2009, inayotoa ufafanuzi kuwa mtoto ni mtu aliye na umri chini ya miaka 18, na kwamba kunazia 18 kwenda juu ni mtu mzima ambaye ana uwezo wa kuamua jambo.
Hivyo, wakati nchi imefikia hatua mbalimbali za kutokomeza ukatili, ni vyema kujua kuwa nguzo muhimu ya kumaliza ndoa hizo ni kuwa mfumo imara wa sheria unaoweka umri wenye uwiano wa kuolewa au kuoa kwa makundi hayo ya jinsi mbili kuwa miaka 18.
Ninaamini kuwa umri ambao umekuwa ukiwekwa na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia, hakutakuwa na ndoa za utotoni na pia watoto wa kike wanaweza kuwa salama zaidi.
Watakuwa salama kwa sababu wanaweza kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI, magonjwa ya zinaa, manyanyaso, athari za kisaikolojia, kimwili na ukatili wa kijinsia kupitia ndoa hizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED