Uchaguzi Mkuu unatukaribisha, wanahabari nasi tuingie hivi...

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 01:36 PM Aug 07 2025
Waandishi wa habari kwenye makumu yao
Picha: UN
Waandishi wa habari kwenye makumu yao

SAFARI ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu inazidi kusonga, wadau kadhaa wanaohusika katika kusimamia ama kuhamasisha jambo hili linafanikiwa wapo kazini.

Katika tasnia ya habari, kuna mambo kadhaa yamejitokeza ambayo pengine yakaonesha tofauti kiasi fulani katika habari kadhaa zinazohusu uchaguzi huu.

Uchaguzi wa mwaka huu unafanyika ukiwa na mambo yanayoweza kuleta mabadiliko chanya. Hayo ni kama vile, 

kukua kwa teknolojia na kufanikisha uwapo wa akili unde (AI), pia kusajiliwa kwa waandishi wa habari kwenye Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).

Hatua ya usajili wa JAB umetajwa kudhibiti watu ambao siyo wanahabari kujihusisha na uandishi wa habari. Hatua hii inatarajiwa kuona habari zinazoendelea kuripotiwa kwenye vyombo vya habari zinakuwa zile zinazozingatia taaluma, ikiwamo ukweli, pia zenye maslahi kwa wananchi.

Kuwapo ‘AI’ au akili unde, kunatajwa kusaidia kuwarahisishia waandishi wa habari, kubaini taarifa sahihi na wakaitumia kwa usahihi.

Niseme, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni miongoni mwa taasisi ambazo zimejitokeza mstari wa mbele kuhakikisha inatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari nchini, ikiwa ni hatua ya kufanikisha taarifa za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kwamba zinakuwa sahihi.

Mnamo Agosti 2 mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, alifungua mkutano wa kitaifa kati ya Tume na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu, Dar es Salaam.

Katika mjumuiko huo, akawataka wataaluma hao wa habari kutumia taaluma zao kuhamasisha na kuwaelimisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Akavitaja vyombo vya habari vina mchango mkubwa kulinda mshikamano wa kitaifa, pia kuimarisha demokrasia  ya ndani, kwa kuripoti taarifa sahihi.

Anasema vyombo vya habari vina wajibu kupitia habari inazoripoti kwamba, zinaelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa INEC Ramadhani Kailima, anawaasa wanahabari akiwataka wahakikishe wanatoa taarifa sahihi kwa wananchi wasishiriki kusambaza taarifa potofu.

Anasema INEC imejipanga katika kuhakikisha inashirikiana kikamilifu na vyombo vya habari, ikiwamo kujitokeza kwa mahojiano au taarifa, akiahidi kutolewa ushirikiano sahihi.

Kuanzia Septemba Mosi hadi 30 mwaka huu, INEC itazindua mfumo wa kusajili vyombo vya habari utakaosaidia kupata vibali kutokana na vitambulisho rasmi vya waandishi watakaoripoti habari za wakati wa Uchaguzi Mkuu

Hatua hiyo ya INEC kufanya mafunzo kwa wahariri na waandishi imekamilisha mikutano yake na wadau tangu Julai 27 mwaka huu.

Ilishakutana na vyama vya siasa, wawakilishi wa wanawake, asasi zisizo za kiserikali, vijana na watu wenye ulemavu.

Pia, Chama cha Waandishi wa habari wanawake nchini (TAMWA) nacho kilitoa mafunzo, ikiwamo kukumbusha matumizi ya akili  unde.

Hiyo ni katika kuhakikisha wanatumia vyema kuepusha taharuki na maumivu kwa wanajamii, kutokana na usambazaji habari potofu, hasa katika mchakatato wa uchaguzi mkuu.  

Mafunzo hayo maalum yalilenga kuwajengea uwezo na ustahimilivu katika zama za kidijitali, yametolewa Dar es Salaam na TAMWA walioshirikiana na taasisi ya kimataifa.  

Mkurugenzi wa TAMWA Dk. Rose Reuben anasema wanalenga kukumbusha wajibu wa mwandishi  katika kuhakikisha anazingatia kufanya kazi zake kwa matakwa ya taaluma ya habari zenye ukweli na uadilifu.

Msisitizo wake msomi huyo wa uandishi, anawasisitiza waandishi kuandika habari zitakazosaidia jamii, akitahadharisha watakaotumia vibaya akili unde, pia taarifa zinazodhalilisha heshima na utu wa watu.

Waandishi wamenolewa katika namna kukabiliana na vikwazo vya mtandao, kwa kufanikisha kuwapo mbadala, ili visikwaze jamii hata wakahabarishwa  kwa wakati uliokusudiwa,.

Mkufunzi wa mafunzo hayo ya wanahabari, Yose Hoza, anasema wamelenga kuwaongezea uwezo wa kulinda vifaa vyao kama simu na laptop, pia kuwajengea uwezo wa kuandaa maudhui yenye maslahi kwa umma.