Wabongo tusingejitendea haki kumpoteza Karia

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:44 PM Aug 18 2025
Wallace Karia
Picha: Mtandao
Wallace Karia

WALLACE Karia, ataendelea kuliongoza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa miaka mingine minne.

Ni baada ya kuidhinishwa kwa asilimia zote na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi uliofanyika Jumamaosi mjini Tanga.

Uchaguzi huo unahitimisha siku 78 tangu ulipotangaza na kuanza kwa mchakato huo, Juni 14 mwaka huu.

Karia ataongoza TFF akiwa na wajumbe sita wa Kamati wa Utendaji waliochaguliwa katika uchaguzi huo, ambao ni Hosea Lugano, Salum Kulunge, james Mhagama, Mohamed Aden, Mrisho Bukuku na Khalid Abeid.

Muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa kishindo kuendelea kuiongoza (TFF), alisema katika uongozi wake hautafanya mambo ya kulipa kisasi ambapo watajipanga kufanya mambo ya maendeleo kwa maslahi ya soka la Tanzania.

Kwanza kabisa nimpongeze, Karia kwa kuchaguliwa tena kuendelea kuiongoza TFF, ambao kusema kweli mpaka sasa imefanya mambo makubwa nchini katika mchezo wa mpira wa miguu chini yake.

Wapo watu ambao walitaka kuhakikisha rais huyo harejei madarakani kwa njia ambazo si za uchaguzi, lakini hazikufanikiwa.

Kuna baadhi ya watu ambao wanaona kama mafanikio haya yote nchini katika nyanja za soka yamekuja tu kama bahati, lakini ukifuatilia na kufanya uchunguzi bila kubebwa na mihemko, utagundua kuwa ni mipango mikakati ya serikali ambayo imekuwa ikishirikiana bega kwa bega na TFF kuhakikisha soka linasonga mbele.

Ukianza kwa mafanikio ya timu za mpira wa miguu za Simba na Yanga kwenye michezo ya kimataifa ni kwamba serikali imeweka mazingira wezeshi kiasi kwamba timu hizo zimekuwa zikisajili wachezaji wa kigeni 12, ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakizisaidia timu hizo kushinda mechi zao hata zinapocheza na timu ambazo zamani zilikuwa sumbufu za Afrika Kaskazini, maarufu kama timu za Waarabu.

Kumekuwa na wadau wa soka ambao walikuwa wanataka wachezaji wa kigeni wapunguzwe wabaki watano tu ili kuwe na wachezaji wengi wazawa kwenye klabu za Tanzania.

Mmoja wa waliopigwa na Rais Karia, ambapo alibainisha kuwa kama lengo ni kuisadia timu ya taifa, yeye anaona uwepo wa wachezaji 12 wa kigeni kwenye timu zetu umewasaidia mno kuwaimarisha wachezaji wa Kibongo, kiasi kwamba hata timu ya taifa ya sasa, Taifa Stars imekuwa imara kuliko wakati mwingine wowote.

Chini ya Rais Karia, ndiyo wakati klabu za mpira zimefanya vyema baada ya muda mrefu sana kupita.

Ndiyo wakati timu ya taifa, imefuzu fainali za Mataifa ya Afrika AFCON mara tatu, 2019, 2023 na 2025, baada ya kufanya hivyo miaka mingi iliyopita, 1980.

Karia na TFF, kwa ushirikaino mzuri wa serikali wamezifanya timu za vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes chini ya miaka 20, pamoja na timu za wanawake kuwa moja ya timu tishio barani Afrika, zikifanikiwa kutwaa makombe katika mashindano mbalimbali, ambapo huko nyuma hatukuwahi kushuhudia hilo.

Ni ukosefu wa shukrani kama hatutoipongeza serikali na TFF chini ya Karia, ambapo kwa mara ya kwanza wameifanya timu ya taifa ya Tanzania ya CHAN kuongoza Kundi B, ikitinga robo fainali kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe 2009 nchini Ivory Coast.

Kusema kweli Watanzania wala tusingejitendea haki, au wajumbe wasingetenda haki kama wasingemrudisha Karia, ili ashirikiane na serikali hii kupeleke mbele gurudumu la soka nchini ambalo kwa sasa linakwenda kwa kasi kama vile lipo mteremkoni.

Uenyeji wa fainali za CHAN unaoendelea nchini na ule ya AFCON 2027 unaonesha dhamira halisi ya dhati ya serikali kuendelea mpira wa miguu nchini.

Tunamtakia Karia kila la heri kwenye kazi yake hiyo, aendelee kushirikiana na serikali kuifanya Tanzania kuendelea  kuwa tishio zaidi kwenye mchezo huo Afrika, kwa klabu za wanaume na wanawake, timu za taifa za wanaume, wanawake na vijana pia.