Wanafunzi mjizoeze zaidi kusoma vitabu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM Sep 03 2025
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Msalato wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za sekta ya sheria na haki za binadamu, Januari 23, 2023
Picha: THBUB
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Msalato wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za sekta ya sheria na haki za binadamu, Januari 23, 2023

WANAFUNZI wako likizo ya ‘mid tem’ lakini kuna wanaomaliza darasa la saba wiki hii. Someni vitabu na majarida pamoja na taarifa mbalimbali kutafuta maarifa mapya huku mkijihadhari na unyanyasaji mitaani.

Ndizo salamu tunazotuma kwa wahitimu wa darasa la saba na wote walioko likizo wakiwamo wanavyuo vikuu ambao watarejea tena shuleni Novemba baada ya uchaguzi mkuu.

Jizatitini kusoma kwani kuna ulazima wa kujifunza na kufundishwa kusoma vitabu badala ya kuendelea kuamini kuwa kusoma na kupenda vitabu ni hobi.

Ni wazi kuwa kama wanafunzi wetu wa ngazi zote hawatapenda kusoma ni wazi kuwa wakifika shuleni au vyuoni kokote watakuwa si wasomaji.

Kuanzia sasa tujilazimishe na kujijengea mazoea ya kusoma vitabu kwenye misimu ya likizo ikiwamo ya kumaliza darasa la saba, ya kuhitimu kidato cha nne, sita na wakati wote ili mapumziko yasiwe hasara.

Watumie muda wao kusoma vitabu vya aina mbalimbali na hata kujibu mitihani kwa njia zozote zile kama wanaweza watumie mitandao.

Wakumbuke kukosa mazoea ya kujisomea vitabu kunaonesha jinsi kulivyo na athari kubwa katika jamii. Kwa wanafunzi wengi kuanzia msingi hadi vyuo vikuu wanakosa kufahamu mambo mengi kwani vitabu vimejaa maarifa.

Ni wazi kuwa kutokusoma kunasababisha kufeli mitihani kutokana na uchache wa maarifa na wakati mwingine wengine kuambulia alama za chini kwenye mitihani hasa vyuo vikuu kutokana na kushindwa kujenga hoja za kuwashawishi wahadhiri kwa kutoa mifano mingi zaidi ambayo angewapatia alama za juu ambazo zinatoka kwenye vitabu na makala mbalimbali.

Wanafunzi wengi hufeli kutokana na uvivu wa kusoma vitabu na kuvielewa, matokeo yake ‘humeza’ vitini ambavyo vimefanyiwa uchambuzi wa vitabu hivyo, hali inayosababisha kutojenga hoja zenye kuwashawishi wasahihishaji ambazo ingekuwa rahisi kwao kama wangesoma vitabu na kuvielewa.

Hata katika muktadha mwingine kama vile kanisani, kwenye warsha na semina mbalimbali,watu wamekuwa wategemezi wa kusikiliza wenzao na si kujisomea wenyewe ili kuelewa zaidi.

Kwenye makanisa, mfano Padri au Mchungaji anaweza kufundisha na kutoa mistari katika Biblia ili watu wakasome na kujifunza zaidi, wengi hawafanyi hivyo kwa kuona uvivu hivyo kubaki na uelewa kidogo kuhusu Neno la Mungu.

Kutopenda kusoma kuna athari nyingi mathalani, kwenye ajira kuna wanaosaini mikataba ya kazi inayowakandamiza kutokana na kutokuwa na mazoea ya kusoma kilichomo.

 Wanapokuja kushtuka baada ya kuona athari za mkataba waliyosaini muda umeshakwenda na hawana la kufanya na kuamua kuacha kazi na kupoteza haki zao kwa uvivu wa kusoma.

Ni ukweli kuwa kama ambavyo jamii yetu ilivyokosa ari ya kujisomea ndivyo na watoto wanavyokosa mwamko na ari ya kusoma, hivyo likizo zitumike kusoma si kubakia mbumbumbu licha ya kwamba wangeweza kufanya jambo la kujiongeza kitaaluma.

Usemi kuwa ‘kuna nguvu kubwa katika kujisomea ’ unamaana pana kwamba kupitia vitabu na majarida mtu anaweza kujifunza vitu mbalimbali kushinda hata vile ambavyo angekwenda shuleni.

Aidha, inamaanisha kusoma vitabu kunampa msomaji elimu na maarifa makubwa hata bila mwalimu. Kwa kifupi mtu anaweza kujitibu bila hata kwenda hospitali, mfano matatizo ya kisaikolojia, vipo vitabu mbalimbali vinavyoelezea jinsi ya kupambana na matatizo ya kisikolojia kwa rika zote.

Katika kujisomea mtu anaweza kujifunza jinsi ya kukabiliana matatizo na vishawishi, mfano unaweza kukutana na safari za maisha za waandishi mbalimbali na jinsi walivyokabiliana na vishawishi, changamoto na shida nyingi lakini wakazishinda.

Mfano, kitabu cha I will, I must, I can’ kilichoandikwa na Dk. Reginald Mengi, kinafundisha vijana na watu wote kusimamia ndoto zao na kuhakikisha zinafanikiwa na kuwafikisha pale wanapotaka, wakikabiliana na changamoto zinazoambatana nao bila kuchoka.

Katika jamii yetu kuna tofauti kubwa ya kifikra na kimtazamo kati ya mtu mwenye utamaduni wa kujisomea vitabu na majarida na yule asiyekuwa na utamaduni huo.

Mwenye kusoma vitabu anajenga hoja nzito yenye mifano hai kwa kuwa anajua vitu vingi na hashindwi mambo. Lakini yule ambaye si wa vitabu utamsikia akiongea maneno yale yale kuwa kenge anaweza kufyoanza ubongo wa binadamu.

Kwa hiyo kinachotokea wakati huu kiwe funzo kuwa tunatakiwa kuanzisha masomo na mitihani ya kusoma vitabu. Taasisi za elimu zianze kufikiria jinsi ya kuwafundisha watoto wetu shuleni na vyuoni kusoma vitabu.

Kwa walioko likizo hawajachelewa hebu watumie muda huu kujifunza na kujizatiti kusoma vitabu hata kama hawajazoea.