Watakaoshinda katika kura maoni wasijivune, wa kushindwa wasinune

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 06:49 PM Jul 24 2025
Tume Huruya Taifa ya Uchaguzi
Picha: Mtandao
Tume Huruya Taifa ya Uchaguzi

“ASIYEKUBALI kushindwa siyo mshindani, “ni msemo wa wahenga wa Kiswahili, ambao kwa namna yake una nafasi kusaida kutuliza maumivu, hasa baada ya matokeo ya ushindani kwenye jambo husika.

Nami nasimamia hapo kwenye mtaa wa wahenga, kwamba katika nafasi hizi za uteule wa vyama siasa, washindi katika kura maoni wasijivune kujiona wamemaliza safari, ukweli wake bado parefu. 

Waliovuka wasijisahau na kujitunisha dhidi ya washindani wa sasa, kwa kuwa mchakato huu mwisho wake mwezi Oktoba ijayo, baada ya upigaji kura kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu, ukihusisha rais, wabunge na madiwani. 

Niwakumbushe wagombea wanaovuka kwamba, hawajafika wanakopatafuta! Uhakika wa kushinda uko mbele, iko katika wigo wa wapiga kura, wananchi wanaomhitaji kiongozi mwenye sifa na uwezo wa kuwawakilisha kuwasilisha kero zinazowakabili na kusaka maendeleo iwe jimbo au kata husika . 

Pia, walioshindwa nao wajitahidi kudhibiti maumivu ya kukwama, wakikubali ukweli “kwenye kushindana, lazima yupo atakayeshinda na atakayeshindwa.” 

Hivyo, hawapaswi kuruhusu roho za vinyongo na chuki kuwatawala au kutumika vibaya, iwe kwenye chama au eneo husika. 

Mchakato unahusu vyama 18 vya siasa vyenye usajili kamili, serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambavyo 12 Aprili mwaka huu jijini Dodoma, walitia saini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.

 Wadau hao ni Chama cha Mapinduzi (CCM), United Peoples’ Democratic Party (UPDP), Civic United Front (CUF), National Convention for Construction and Reform (NCCR), National League for Democracy (NLD), Tanzania Labour Party (TLP), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA) na Union for Multiparty Democracy (UMD).  

Vyama vingine ni National Reconstruction Alliance (NRA), Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), United Democratic Party (UDP), Madini Kilimo Nishati (MAKINI), Democratic Party (DP), Alliance for African Farmers Party (AAFP),  Sauti ya Umma (SAU), Chama cha Kijamii (CCK), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na  Alliance for Democratic Change (ADC) . Mchakato huo umekuwa na taarifa za baadhi ya wagombea kutumia mbinu chafu, ikiwamo utoaji rushwa kwa baadhi ya wajumbe. 

Ni wazi watu kama hawa  wakipita kwenye hatua hii, ni hatari kwa maendeleo ya jamii, kwa kuwa watashughulika kujitafutia fedha kinyume na utaratibu, ili mradi kufidia gharama walizotumia kusaka ushindi. 

Nasema washindi kwa namna hiyo wakipata nafasi ya kupenya katika uchaguzi, maana yake ni kwamba ipo siku watavifedhehesha vyama vyao. 

Hiyo ni kutokana na kwamba, licha ya uwapo kwa kanuni zinazopaswa kuzingatiwa kwenye vyama ili kufanikisha mchakato wa uteuzi wa wagombea husika, ikiwamo kuepuka vitendo vya rushwa. 

Uzoefu unaonesha kuwa wapo, wasiokuwa tayari kuzingatia hayo,  wanachozingatia ni maslahi yao binafsi.   

Naamini wananachi wapenda maendeleo, wanatamani kuona Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zinazingatiwa, kuhakikisha usahihi katika mchakato wote wa tendo hilo. 

Umewekwa muda kutumika kwa Kanuni za Maadili. Kanuni hizo za maadili, zitatumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kuanzia siku moja baada ya tarehe ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mkuu hadi baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo. 

Vilevile, inalaezwa kuwa ni kanuni zitakazotumika katika chaguzi ndogo zitakazofuata, baadaye. 

Ni wazi kwamba, wananchi wengi wanatamani kuona mchakato mzima wa uchaguzi Mkuu kwa ujumla unakwenda vizuri, ikiwamo ushindani halisi, badala ya kutumika kwa njia yoyote ya udanganyifu, pia kudhibitiwa kwa wanasiasa waroho wa madaraka wasiokubali kushindwa, bali hujiaminisha kuwa washindi. 

Hao tunawafahamu tabia zao, hutumia njia chafu ikiwamo kueneza chuki ili kusababisha uvunjifu wa amani nchini. 

Hivyo narudia kwamba, watakaoshinda wasijivune, bali wajipange vyema kuhakikisha wanashiriki kusaidia wananchi kusaka maendeleo na kutafuta njia bora ya kutatua kero zao. 

Watakaoshindwa wawe na moyo wa uvumilivu, hata ikiwezekana wajitahidi kushirikiana na walioshinda kuwasilisha mawazo yao ya kufanikisha huduma bora kwa jamii badala ya kununa na kususa.