Tanzania, DRC zaweka mikakati kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:21 PM Apr 24 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Tanzania, DRC zaweka mikakati kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, amekutana na Waziri wa Utalii wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Didier M'Pambia, kujadili njia za ushirikiano katika kukuza sekta ya maliasili na utalii kati ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Jukwaa la Pili la Kimataifa la Utalii wa Vyakula (2nd UNWTO Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) linaloendelea leo, Aprili 24, 2025, katika Hoteli ya Gran Meliá, jijini Arusha, chini ya uratibu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO).

Katika kikao hicho, viongozi hao walijadiliana kuhusu fursa za ushirikiano katika masuala ya utalii wa mipakani, utalii wa kiikolojia (eco-tourism), pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kwa ajili ya kuinua mchango wa sekta ya utalii kwenye uchumi wa mataifa yao.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nkoba Mabula, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Thereza Mugobi, Mkurugenzi Msaidizi,Richie Wandwi, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Wizara ya Utalii ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kukuza utalii kama kichocheo cha maendeleo endelevu kwa pande zote mbili.