Afariki dunia akigongwa na mfuniko mtungi kuzimia moto

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 01:29 PM Oct 19 2025
Mtungi ambao mfuniko umefyatuka na kusababisha kifo
Picha: Julieth Mkireri
Mtungi ambao mfuniko umefyatuka na kusababisha kifo

MTU mmoja amefariki dunia baada ya kupigwa kichwani na mfuniko wa gesi ya kuzimia moto, huko Masiwa, kata ya Dunda, wilaya ya Bagamoyo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, katika taarifa yake aliyoitoa Oktoba 18, 2025, ofisini kwake Kibaha, mfuniko huo wenye uzito ulifyatuka kwa kasi, baada ya kupigwa na nyundo.

Kamanda Morcase amesema mfuniko huo baada ya kufyatuka ulienda kumpiga Mengi Waziri (25), aliyekuwa umbali wa mita 10, akiendelea na shughuli zake na ilimsababishia kifo.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo umebaini kijana Musa Rashid (19), muokota vyuma chakavu, alikuwa akigonga mfuniko huo wa mtungi  kwa nyundo, ili aufungue.

Kamanda amesema ghafla mfuniko huo uliruka kwa kasi na kwenda kumgonga kichwani Mengi na kumsababishia kifo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Bagamoyo, ukisubiri taratibu za kitabibu.

Jeshi la Polisi, limetoa tahadhari kwa wananchi wanaookota na kuuza vyuma chakavu, kuacha tabia ya kugonga au kukata vitu ambavyo vinaweza kusababisha mlipuko.