MAHUJAJI wanaotarajiwa kufanya ibada ya hijja nchini Saud Arabia kwa mwaka 2026 ambao wana tatizo la tezi dume na ngiri, wametakiwa kufanya upasuaji mapema kabla ya safari hiyo.
Hayo yamesemwa leo, visiwani Zanzibar na Daktari Dhamana, Afya za Mahujaji kutoka Ofisi ya Hijja ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Naufal Kassim Mohammed, kufuatia agizo na maelekzo ya serikali ya Saud Arabia, kuhusu afya za mahujaji kwa mataifa yote duniani yanayosafirisha mahujaji ikiwemo Tanzania.
Amesema ikiwa hujaji atashindwa kufanya upasuaji kabla ya safari hataruhusiwa kusafiri kwenda kutekeleza ibada hiyo.
Aidha daktari huyo amesema pia wanaosumbuliwa na maradhi ya figo yanayohitaji kufanyiwa usafishaji, maradhi ya moyo yanayomzuia mtu kufanya shughuli zake za kawaida na wenye ugonjwa wa mapafu unaohitaji matumizi ya oksijeni, hawataruhusiwa pia.
Aliyataja maradhi mengine ni ugonjwa wa ini, uti wa mgongo yanayomzuia mtu kufanya shughuli za kawaida, maradhi ya mishipa ya fahamu yanayopelekea ulemavu wa viungo, uzee, afya ya akili, ujauzito, maradhi ya miguu yanayosababisha kumzuia mtu kutembea kwa muda marefu na wagonjwa waliopo kwenye matibabu ya saratani.
Daktari huyo amesema ni vyema taasisi zinazosafirisha mahujaji kufuata miongozo inayotakiwa, kufuatwa, ikiwamo mahujaji wapimwe afya zao pale tu wanapojiandikisha na kufanya maamuzi kuwa aliyejiandikisha ataweza safari ya hija au laa.
Hata hivyo amesema kuwa maelekezo na muongozo huo umekuja kufuatia kuwapo kwa changamoto nyingi za kiafya, kwa mahujaji waliotekeleza ibada ya hija nchini Saud Arabia, huku ikisisitizwa kuwa mahujaji kupata chanjo ya homa ya ini, uti wa mgongo, manjano na polio.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED