Othman aahidi ajira bila upendeleo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:19 AM Oct 19 2025
Othman aahidi  ajira bila upendeleo
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Othman aahidi ajira bila upendeleo

Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kwamba katika Serikali atakayoiongoza, kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) haitakuwa tena kigezo cha kupata ajira, bali uwezo, uadilifu na uzalendo kwa taifa ndivyo vitakavyotumika kama msingi wa ajira.

Akihutubia mamia ya wananchi wa Shehia ya Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Othman alisema moja ya matatizo makubwa yanayoikumba Zanzibar ni ukosefu wa uadilifu Serikalini, unaosababishwa na tabia ya kupeana kazi kwa upendeleo na misingi ya kisiasa.

Alisema Serikali imegeuzwa kuwa kama duka la mafisadi, ambapo kazi hazitolewi kwa uadilifu bali kwa kujuana na kuwa na kadi ya CCM. Huu ni unyanyasaji mkubwa kwa vijana wanaostahili nafasi hizo kwa juhudi zao.

Amesisitiza kuwa katika Serikali ya ACT Wazalendo, watumishi wa umma watabaki huru kisiasa na hawatalazimishwa kujiunga na chama chochote ili kulinda heshima ya taaluma na maadili ya utumishi wa umma.

Aidha, Othman alizungumzia sekta ya utalii, akisema licha ya kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar, sekta hiyo imeanza kuchafua maadili ya jamii kutokana na baadhi ya watalii kutovaa mavazi yenye staha na kukiuka mila na desturi za Kizanzibari.

Alisema watalii wanapaswa kuja Zanzibar wakiheshimu mila zetu, sio kuzunguka mitaani nusu uchi na kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ya Wazanzibari. 

Aliongeza kuwa Serikali yake itahakikisha watalii wanaelimishwa kabla ya kuingia mtaani. Othman pia alionya juu ya tabia ya kujenga mahoteli ya kitalii kila mahali bila mpangilio, akisema hali hiyo inaathiri mazingira na ustawi wa jamii.

 Ameeleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya ACT Wazalendo ya mwaka 2025 imetoa mwelekeo wa kulinda rasilimali za nchi na kuendeleza utalii wa heshima unaonufaisha wananchi.

Kuhusu ajira, Othman aliahidi kwamba vijana wataajiriwa bila ubaguzi na pia watapatiwa fursa nyingi za kujiajiri kupitia ujasiriamali, huku Serikali ikitengeneza mazingira rafiki kwa maendeleo ya biashara ndogo ndogo na miradi ya kiubunifu.

Alisema Serikali atakayoiongoza itajengwa juu ya misingi ya uadilifu wa kweli, itakayoweka mbele uwezo wa mtu na sio chama chake. Vijana watakuwa sehemu ya mabadiliko haya.