Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa ametoa tahadhari kwa wananchi mkoani humo hasa vijana kutoshiriki kwenye vurugu za aina yoyote ambazo zinapangwa kufanyika siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu.
Amewataka kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu ili taifa liendelee kupata maendeleo kwenye sekta mbalimbali.Ametoa tahadhari hiyo aliposhiriki kwenye usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya na mbio za pole (Jogging), zilizoandaliwa na vilabu vya mbio hizo jijini humo.
Amesema serikali itasimamia na kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila kuwepo kwa rapsha za aina yoyote na hivyo akawataka wananchi kutoogopa kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura.
“Mtu yeyote asije akaanza kujifunza kufanya fujo siku ya uchaguzi, nadhani lengo letu hapa ni kuhamasishana kushiriki uchaguzi kwa amani, kwahiyo naomba mkatusaidie kuhamasisha na watu wengine wasishiriki kufanya fujo,” alisema Malisa.
Mwenyekiti wa Chama cha Vilabu vya mbio za pole jijini Mbeya, Abuu Mtoro amesema moja ya dhamira ya mbio hizo ilikuwa ni kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye uchaguzi mkuu pamoja na kutunza mazingira ili kuepuka magonjwa.
Amesema vijana ndio waliokuwa wanalengwa Zaidi kushiriki kwenye shughuli hizo na kwamba wamejitokeza na ujumbe uliokuwa unalengwa kuwafikia uliwafikia kutokana na ushriki wa viongozi mbalimbali wa serikali.
Amesema mbali na wanachama wa vyama vya mbio za pole, pia wameshiriki wataalamu wa masuala ya afya kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi na kutunza mazingira kwa ajili ya afya zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED