MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amerejea nyumbani kwao wilayani Nyasa mkoani Ruvuma na kupokelewa kwa matukio ya kimila na wazee.
Dk. Nchimbi amewasili leo Oktoba 19 katika Kata ya Lituhi Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, pamoja na mambo mengine alipokelewa na wazee kisha kufanyiwa matukio kadhaa ya kimila yakiashiria kumkaribisha na kumpa baraka katika uongozi.
Akiwa katika Uwanja wa Kata ya Lituhi, matukio ya kumkaribisha kimila Dk. Nchimbi na kumpa baraka yaliongozwa na Chifu wa Nyasa na Katibu wa machifu wa Mkoa wa Ruvuma, Saad Wabu Musa.
Matukio aliyofanyiwa Balozi Dk. Nchimbi ni pamoja na kuzungushiwa unga wa mhogo, kuita kuita mizimu kuashiria kwamba mtoto (Dk.Nchimbi) amerudi nyumbani.
Tukio lingine ni Balozi Dk. Nchimbi kuvalishwa shuka (mgolole), kupewa mkuki na ngao, kukaa katika kigoda, kufungwa kitambaa chekundu kwenye paji la uso kuashiria kwamba ufalme unatoka nyumbani na kwenda serikalini.
ATOA SHUKRANI
Baada ya kufanyika kwa matukio hayo, Balozi Dk.Nchimbi alisema: "Nawashukuru wazee wa kimila Nyasa kwa heshima mliyonipa ya kuwa mmoja wa viongozi wa kimila. Nawahakikishia wazee wangu nitafanya kila jitihada kumsaisia Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza Ilani ya CCM".
Kadhalika ameaema atafanya jitihada za kumwaminisha Rais Samia Suluhu Hassan asijutie kumchukua mtu kutoka mkoani Ruvuma kuwa msaidizi wake.
Balozi Dk. Nchimbi amesema endapo (yeye) akimpa msaada dhaifu Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa amewaangusha wananchi wa Ruvuma na Kusini, kwamba atafanya jitihada ili asiwaangushe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED