Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imepokea rasmi karatasi za kura zilizochapishwa na Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZGP), ikiwa ni hatua muhimu katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo leo, Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabit Idarous Faina alieleza kuwa mchakato wa kupata mzabuni ulifanyika kwa umakini mkubwa kupitia utaratibu maalum wa zabuni uliofanya tathmini ya viwanda vinne vya uchapaji ambavyo ni Lebone Litho Printers (PTY) Ltd,UniPrinter iliyopo Durban Afrika Kusini,Kampuni ya nchini China ya Electronics Shenzhen Company (CES) na Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZGP).
Baada ya tathmini hiyo, Tume iliamua kumpatia zabuni Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZGP) kutokana na ubora wa huduma, uzoefu, viwango vya kiusalama vya uchapaji na ukaribu wa usimamizi wa kazi hiyo.
Aidha,Mkurugenzi Faina amesema kuwa,gharama za uchapaji zilikuwa Shilingi 908,327,300 wakati bajeti iliyokuwa imetengwa awali ilikuwa Shilingi 1,245,592,000, jambo linaloonyesha kuwa kazi hiyo imefanyika kwa gharama nafuu bila kuathiri ubora.
“Hii ni dalili ya matumizi bora ya rasilimali za umma na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa,” amesema Mkurugenzi Faina.Amesema kupokelewa kwa karatasi hizo za kura ni ishara ya hatua muhimu kuelekea maandalizi ya vifaa vyote vya Uchaguzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED