Watanzania watakiwa kutumia mkaa mbadala

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 11:11 AM Oct 19 2025
Watanzania watakiwa kutumia mkaa mbadala
PICHA: PAUL MABEJA
Watanzania watakiwa kutumia mkaa mbadala

Kutoka na kuongezeka kwa athari za mabadiliko tabianchi nchini Watanzania wametakiwa kuacha matumizi ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia, na badala yake watumie nishati safi ikiwamo mkaa mbadala ili kulinda afya zao pamoja na mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Foundation For Disabilities Hope (FDH) Maiko Salali, amesema hayo leo  Oktoba 19,2025, wilayani Mpapwa mkoani Dodoma, wakati akitoa elimu ya matumizi ya mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes unaozalishwa na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO).
Salali, amesema matumizi ya nishati chafu nchini hivi sasa imekuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti ovyo kwa ajili ya nishati ya kupikia.
“Matumizi ya nishati chafu ya kupikia hasa kuni na makaa yanaleta madhara ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira nchini hivyo tunahimiza matumizi ya mkaa huu mbadala ili kusaidia kulinda uhifadhi wa mazingira pamoja na afya za Watanzania,”amesema
Amesema Tanzania na Dunia zimeweka mkakati kukabiliana na hali hiyo kwa kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya nishati chafu ya kupikia kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kuhusu mkaa huo, amesema licha ya kulinda afya na mazingira pia ni sehemu ya watu kujikwamua kiuchumi kwa kuomba uwakala wa kuuza nisahti hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Sisi kama taasisi ambayo inajihusisha pia na kusaidia watu wenye ulemavu tumepatiwa uwakala na STAMICO, kwa ajili ya kusambaza bidhaa hii hivyo kusaidia kundi la watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi waliokuwa nao hapo awali,”amesema Salali
Alisema pia mkaa huo ni rafiki kwa watu wenye ualibino ambao ngozi zao zinaathirika kutokana mionzi ya jua itokanayo na uktaji miti ovyo na kuwa sababishia kupata saratani ya ngozi.

Tafiti zinaonesha kuwa watu 30,000 hufariki kila mwaka nchini kutokana na magonjwa mbalimbali wanayoyapata kwa sababu ya kutumia nishati chafu ya kupikia ikiwemo kuni na mkaa.
Kutokana na ukataji miti kwa matumizi ya kuni na mkaa kumekuwa na athari nyingi katika afya kwa mtumiaji hasa mtoto na mwanamke ambaye muda mwingi anakuwa jikoni hali inayosababisha mfumo wake wa upumuaji huathirika.