NHIF yaridhia Hospitali Aga Khan kutisha huduma kwa wanachama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:08 AM Aug 12 2024
Hospitali ya Aga Khan.
Picha: AKDN
Hospitali ya Aga Khan.

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeridhia ombi la Hospitali ya Aga Khan kusitisha huduma za matibabu kwa wanachama wa mfuko huo kuanzia kesho kutokana na sababu za kiuendeshaji.

Taarifa ya NHIF iliyotolewa jana na Grace Michael, Kaimu Meneja Uhusiano wa mfuko huo, ilibainisha kuwa kwa mujibu wa mkataba wa mfuko na mtoahuduma, upande wowote unayo haki ya kuomba kusitisha au kuendelea na utoaji huduma.

"Hivyo, Aga Khan kama ilivyo kwa vituo vingine, anao uhuru wa kutumia haki ya kimkataba. Wakati majadiliano na mtoahuduma yakiendelea kuhusu maombi yake ya kusitisha huduma, mfuko unatoa taarifa kwa wadau wake kuwa ifikapo tarehe tajwa hapo juu, wanachama wanashauriwa kutumia vituo mbadala vilivyosajiliwa na mfuko kupata huduma za matibabu.

"Mfuko umesajili zaidi ya vituo 9,000 ambavyo vinamilikiwa na serikali, taasisi binafsi na mashirika ya dini. Vituo hivyo ni vya ngazi mbalimbali kuanzia zahanati hadi ngazi ya Hospitali ya Taifa ya Rufani. 

"Lengo la kusajili vituo hivyo ni kumpa uhuru mwanachama kuchagua kituo cha kupata huduma za matibabu popote alipo ndani ya nchi," alisema Grace katika taarifa yake hiyo.

Aliongeza kuwa mfuko umefanya maandalizi ya kuwezesha mwendelezo wa huduma kwa wanachama waliokuwa wanapata huduma katika Hospitali ya Aga Khan ikiwamo kusajili vituo mbadala vyenye hadhi sawa au zaidi ya hospitali hiyo.

"Ofisi za NHIF nchini pamoja na Kituo cha Mfuko cha Huduma kwa Wateja zimejipanga kuhakikisha wanachama hawakosi huduma katika kipindi cha mpito.

"Hivyo, endapo mwanachama atapata changamoto yoyote, awasiliane na mfuko kupitia ofisi zake zilizoko nchi nzima pamoja na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachofanya kazi saa 24 kila siku kupitia namba 199 bila malipo," alisema Grace.