Jeshi la Polisi nchini limesema linafanya uchunguzi kufuatia taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ametekwa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, DCP David Misime, amesema jeshi hilo limeona taarifa hizo zinazodaiwa kusambazwa na ndugu wa Polepole, na tayari limeanza kuzifanyia kazi ili kubaini ukweli wake.
Kwa mujibu wa Misime, jeshi hilo lilimtaka Polepole kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusu tuhuma mbalimbali alizotoa kupitia mitandao ya kijamii.
“Polepole alitumiwa barua ya wito kwa mujibu wa sheria za nchi ili aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, lakini hadi sasa hajatekeleza maelekezo hayo,” amesema Misime.
Wakati huo huo, video inayosambaa mitandaoni inaonyesha mtu aliyejitambulisha kama Agustino Polepole, akidai kuwa kaka wa Humphrey Polepole, akisema kuwa ndugu yake ametekwa usiku wa kuamkia Oktoba 6, 2025.
Pia, video nyingine imeonekana ikionyesha sakafu yenye michirizi ya damu inayodaiwa kuwa ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi Polepole kabla ya kutekwa, ingawa uhakika wa video hizo haujathibitishwa rasmi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED