Rais Samia akitaka kiwanda kuimarisha mifumo usambazaji mbolea

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 10:05 AM Jun 29 2025
Rais Samia akiwa na Rais Ndayishimiye wa Burundi wakati wa uzinduzi wa kiwanda huko Nala mkoani Dodoma
PICHA: RENATHA MSUNGU
Rais Samia akiwa na Rais Ndayishimiye wa Burundi wakati wa uzinduzi wa kiwanda huko Nala mkoani Dodoma

RAIS Dk Samia Suluhu Hassan,ametoa raia kwa uongozi wa kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM kuhakikisha kuwa wanaimarisha mifumo ya usambazaji wa mbolea nchini ili iweze kuwafikia wakulima waliopo vijijini.

Ametoa rai hiyo jana jijini Dodoma wakati akizindua na kufungua Kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM  kilichopo Nala, Jijini Dodoma,chenye uwezo wa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka.

“Nitoe rai kwa uongozi wa kiwanda cha ITRACOM hakikisheni kwamba mnaimarisha mifumo ya usambazaji wa mbolea hadi kwa wakulima waliopo vijijini waweze kuipata mbolea hiyo kwa gharama nafuu,"alisema Rais Samia.

Aidha Rais Samia  amezitaka mamlaka za mikoa na serikali za mitaa kutoa elimu ya kina kwa wakulima juu ya matumizi sahihi na vipimo vya mbolea ya FOMI katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Amesema kuwa inawezekana wakulima wakafikiwa na mbolea hiyo lakini wasiwe na maelekezo sahihi ya namna ya kuitumia,huku  akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu ili kuhakikisha mbolea inatumika kwa tija na kwa kuzingatia viwango vinavyofaa kwa kila aina ya zao na ardhi husika.

Hata hivyo ameongeza kuwa kwa kutoa elimu hiyo,kiwanda hicho kitakuwa kimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama wa chakula,kupunguza umasikini na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.

“Kiwango cha biashara kati ya Burundi na Tanzania kinaendelea kukua hivyo uwekezaji huu unaongeza fursa za ajira kwa vijana wetu, na kupitia mpango wa kuongeza vituo vya uuzaji wa pembejeo, wakulima sasa wanapata vifaa kwa gharama nafuu,"amesema Dk Samia.

Amesema serikali imeanzisha pia mpango mkakati wa kujenga mabwawa ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa mvua lengo NI kuzidi kutanua WiFi wa kilimo cha umwagialiaji hapa nchini.

Waziri wa Kilimo,  Hussein Bashe amesema wamekubali kuitwa machawa wa Tanzania kwa kuwasemea ukweli wananchi ili kuhakikisha wanapata fursa za maendeleo zinazotolewa na serikali.

Bashe amesema hayo jana jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Itracom uliofanywa rasmi na Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika eneo la Nala.

Bashe amesema watu wengi wanapenda kuwaita watu machawa pale wanaposema ukweli kitu ambacho wao wamekikubali kutokana na kwamba wanahitaji kuona watanzania wananufaika na fursa zinazotolewa na serikali.

"Tumekubali kuitwa machawa wa Tanzania kwa sababu ya kuwasemea ukweli wananchi kwa serikali na hatutachoka,"amesema Bashe.