KILA kona sasa ni kilio. Ndivyo ilivyo katika nchi kutokana na kuadimika kwa sukari kwenye soko nchini na pale inapopatikana bei yake haishikiki. Katika baadhi ya maeneo, bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya kila siku inauzwa kati ya Sh. 5,000 na 6,000 kwa kilo.
Suala la kuadimika kwa bidhaa hiyo ambayo hutumika kwa masuala mbalimbali yakiwamo kifungua kinywa, na kutengeneza vyakula na vinywaji, lilianza kama mzaha lakini sasa limekuwa sugu. Kuwapo kwa tatizo hilo ni tofauti na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali kwamba upungufu wa sukari utakuwa historia baada ya Kampuni ya Sukari ya Bagamoyo na Kiwanda cha Mkulazi mkoani Morogoro kukamilika.
Katika miaka kadhaa iliyopita, bidhaa hiyo iliadimika katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha serikali, chini ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya msako katika maghala ya wafanyabiashara na kukamata tani nyingi zikiwa zimefichwa. Pamoja na kupatikana katika maghala, sababu nyingine iliyotolewa ni kwamba baadhi ya viwanda vinavyozalisha bidhaa vilikuwa vimefungwa kwa ajili ya ukarabati ikiwa ni maandalizi ya uzalishaji katika msimu mpya unaofuata.
Aidha, serikali ilitoa tamko kwamba pamoja na kuadimika na kufungwa kwa viwanda kama ilivyoelezwa na wamiliki, kiwango kinachozalishwa nchini ni kidogo kulinganisha na mahitaji halisi katika soko.
Kutokana na sababu hiyo, ilielezwa kuwa serikali inatafuta suluhisho la kudumu la kuhakikisha sukari inapatikana kwa ajili ya kutosheleza soko la ndani pamoja na kuwapo kwa ziada ambayo itasaidia kupunguza makali pindi kunapokuwa na upungufu.
Miongoni mwa mipango iliyobainishwa na serikali ni upanuzi wa viwanda vilivyokuwapo kwa wakati huo vya Kilombero, Kagera, Mtibwa na Kilimanjaro (TPC). Pia iliweka bayana kuwa ujenzi wa viwanda vya Bagamoyo na Mkulazi pia vitakapoanza uzalishaji vitapunguza tatizo, hivyo wananchi kupata bidhaa kwa urahisi na kwa bei nafuu.
Licha ya kiwanda cha Bagamoyo ambacho kinamilikiwa na kundi la Kampuni za Bakhresa kuanza uzalishaji na Mkulazi kikiwa katika hatua za mwisho za kuanza uzalishaji, uhaba wa sukari umekuwa mkubwa zaidi na kuwa anasa kwa wananchi wa kawaida kutokana na bei yake kupaa maradufu.
Kuwapo kwa hali hii kunaibua maswali mengi ambayo baadhi yanakosa majibu ya moja kwa moja na matokeo yake wananchi wengi wanaumia ama kwa kukosa sukari au kushindwa kumudu bei iliyoko sokoni kwa sasa. Mbali na hiyo, hivi sasa katika maeneo mengi, mkoa wa Dar es Salaam ukiwamo, bidhaa hiyo haipatikani. Katika siku mbili zilizopita, wananchi wamekuwa wakiisaka bidhaa hiyo madukani, kutoka duka moja hadi lingine, huku majibu wanayopewa ni kwamba haipo.
Suala la viwanda kukarabatiwa ni la kila mwaka na sukari imekuwa ikipatikana na kama ni kwa upungufu si kama wa mwaka huu. Jambo la kujiuliza ni je, Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) na Wizara ya Kilimo hawajui kama kuna uwezekano wa kuwapo kwa upungufu au kuadimika kwa bidhaa hii? Kama wanajua ni hatua gani wamechukua ili kuhakikisha wananchi hawapati adha kama ilivyo sasa?
Pamoja na kuwapo kwa maswali hayo ambayo ni vigumu kupata majibu, jambo la faraja ni kwamba serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, imetamka kuwa tatizo hilo linatarajiwa kumalizika ifikapo Februari 15, mwaka huu. Amesema kumalizika kwa tatizo hilo kunatokana na kutoa vibali vya kuagiza kutoka nje.
Kuna msemo kwamba kila siku binadamu anajifunza kutokana na makosa au uhalisia wa mambo katika maisha ya kila siku. Ni vyema funzo likatolewa na kupata mbinu za kutatua tatizo hilo pindi litakapojitokeza siku zijazo badala ya kuacha wananchi wakaumia mara kwa mara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED