KILA uchao, mitandao ya kijamii imekuwa ikipigiwa kelele duniani kuwa imekuwa ikitumika kwa udhalilishaji watoto na wanawake kwa kuchapisha taarifa na picha kwa lengo la kuwakashifu na kuwachafua katika jamii.
Naamini matukio hayo yanayochangiwa na watumiaji wenyewe wa mitandao hiyo. Mathalani, mtu anaposti picha yake, mkewe na hata mtoto tangia akiwa mdogo na kuweka ‘comment’ (maoni) yake, akijisifia bila kuangalia maudhuhi ya picha yenyewe kuanzia mavazi, mwonekano na mambo mengine.
Mitandao ya kijamii ni hudumua ambayo watu nchini na kwingineko ulimwenguni, hutumia kama njia ya kuwasiliana moja kwa moja kwa kuongea.
Imekuwa ikipigiwa kelele hasa na viongozi kuwa imekuwa ikitumika ndivyo sivyo kwa kusambaza uzushi, taarifa mbaya na potofu kwa lengo la kuchafuana na kuipotosha jamii.
Pamoja na mitandao hiyo kutumika kuunganisha watu kwa nia ya kuhabarishana mambo yanayoendelea kutokea duniani, ikiwamo siasa, michezo, sanaa pia imekuwa ikilalamikiwa kwa kusambaza picha za utupu ambazo zimekuwa zimejaa udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.
Twende mbele, turudi nyuma, hayo mambo kabla ya kuanzishwa kwa mitandao hiyo kama yalikuwepo yalikuwa ni nadra sana.
Ni kumi kwa mmoja, malalamiko hayo yalikuwa yakisikika ya kuwepo kwa vitendo hivyo, hiyo inatokana na kutokuwapo kwa teknolojia ya kisasa na mambo ya utandawazi yanayosababishwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kutokea duniani.
Zama hizo kama ni kuchafuana kulikuwa kwa njia ya mtu kuviziwa kupigwa picha kwa lengo fulani na kuzidurufu kisha kusambaza katika maeneo yaliyokusudiwa kufikisha ujumbe dhidi ya mtu aliyechafuliwa, ikwemo kwenye baadhi ya machapisho, sehemu anakoishi, ofisini na ambako anafanyia shughuli za kujiingizia kipato.
Kwa wakati huo, ilikuwa njia rahisi kudhibiti vitendo hivyo kwa mfano kama kwenye machapisho, mtu aliyelengwa katika tukio hilo, aliweza kufungua kesi ya kukashifiwa mahakamani na kudai fidia.
Hatua hiyo kwa namna moja au nyingine, ilisaidia kuogofya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo na huenda ikawa sababu ya kufanyika kwa namna nyingine kwa kusambaza picha tu mitaani.
Lakini tangu kuanza kutumika kwa mitandao hiyo, kumekuwapo malalamiko ya watu kuchafuliwa kupitia mitandao hiyo.
Katika siku za hivi karibuni, kila kukicha kumekuwa na taarifa zikiwanukuu viongozi wa serikali, siasa na wa dini wakikemea vitendo hivyo vya udhalilishaji hasa vikiwalenga wanawake na watoto.
Malalamiko hayo yanatokana na mitandao ya kijamii kutumika kutengeneza katika ukurasa kwa njia ya maelezo na picha kuhusu makundi hayo kuhusiana na mambo yasiyofaa kwa lengo la kuichafua.
Baadhi ya mitandao ya kijamii maarufu Facebook, Instagram na Twitter, lengo la kuanzishwa kwake ilikuwa ni kusaidia kuongeza kasi ya mawasiliano ulimwenguni.
Nayo matumizi ya simu za mkononi yamekuwa na kasi ya aina yake katika kupeana ujumbe kupitia mitandao hiyo na kusambaziana picha mbalimbali, zikiwamo zisizofaa baadhi zikiwa ni za wanawake na watoto kudhalilishwa.
Naamini matukio hayo yanayochangiwa na watumiaji wenyewe wa mitandao hiyo. Mathalani, mtu anaposti picha yake, mkewe na hata mtoto tangia akiwa mdogo na kuweka ‘comment’ (maoni) yake, akijisifia bila kuangalia maudhuhi ya picha yenyewe kuanzia mavazi, mwonekano na mambo mengine.
Wengine unakuta wametupia picha hizo kwenye ‘status zao’ (hadhi) na zinapoanza kusambaa zinakwenda kwa maudhuhi tofauti.
Hivyo jamii inapaswa kuelimishwa madhara ya kutupa picha kwenye mitandao, kwani kutasaidia kuacha kukurupuka kwa kuiga tamaduni za wenzetu.
Jamii inatakiwa kuelimisha kutumia mitandao hiyo hasa ‘simu janja’ kwa lengo la kupata elimu, biashara, matangazo ya biashara, siasa, ajira, afya, matibabu na utawala.
Mitandao hiyo pia imekuwa ikilalalamikiwa kupunguza ufanisi kazini ofisini kutokana na waajiriwa kupoteza muda mwingi kuchati.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED