Wageni 250 wanatarajiwa kushiriki katika utoaji Tuzo za Utalii Duniani Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi kwa mwaka 2025 (World Travel Awards 2025) huku Tanzania ikiingia kwenye kinyang’anyiro vipengele 50.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana amesema “Hafla ya tuzo hizi itafanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam, kama nchi kwa ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi tumeingia katika kinyang’anyiro hiki katika vipengele 50 kupitia vivutio, huduma bora pamoja na ukarimu wetu kwa watalii.”
Amebainisha kuwa hatua hiyo ni uthibitisho wa hadhi kubwa ambayo nchi imejipatia kimataifa katika Sekta ya utalii na matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa kinara wa kutangaza Utalii kupitia filamu mbalimbali ikiwamo The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Ametaja tuzo zinazoshindaniwa na WTA ni pamoja na eneo bora kwa Utalii Afrika, Bodi bora ya Utali, Kivutio Bora cha Utalii Afrika, Hifadhi bora zaidi Afrika, Kampuni Bora za Utalii, Hoteli inayotoa Huduma Bora kwa Watalii pamoja na Kampuni Bora ya Huduma za Safari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED