JOTO la uchaguzi linazidi kupanda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa wagombea wanaochuana kwenye majimbo mbalimbali, huku kukiwa na taswira tofauti ya wananchi wa miaka ya 90 na wasasa ambao wanahoji wagombea bila woga.
Kwa sasa walioomba kupeperusha bendera ya CCM kwenye majimbo wanatembea kwa wajumbe na wananchi kujinadi kwa uwazi, kisha wanaulizwa maswali na kuyajibu kwa umma.
Kwenye majimbo mengi wagombea hasa waliokuwa wabunge kwa kipindi kimoja na kuendelea wamejikuta kwenye wakati mgumu wa kujieleza sana, kuchekwa, kuzomewa na kuulizwa maswali magumu na wananchi au wanaCCM.
Baadhi ya maeneo wananchi waliohudhuria mikutano husika wameshindwa kuficha hisia zao dhidi ya mgombea fulani, kwa kumweleza wazi hatukutaki! au kuzomea wakati anaongea hadi kuwalazimu viongozi wa CCM wanaoongoza kundi la wagombea kuwatuliza.
Mara kwa mara viongozi wa serikali na CCM wamezungumzia umuhimu wa wananchi kuwahoji wagombea kujieleza kwanini wanataka nafasi ya uongozi, lakini kama alikuwa madarakani ahojiwe ahadi alizotoa mwaka 2020 wakati naomba nafasi hiyo, alizotekeleza na anajipanga kutekeleza nini akipewa nafasi nyingine.
Bila kujali vyeo walivyonavyo wagombea husika, wananchi wameuliza maswali na wengine kupaza sauti kuonesha hawaridhishwi na baadhi ya wagombea hasa walioshika nafasi hizo kwa muda mrefu au kwa kipindi kimoja.
Wapo ambao kila walipokwenda wameshangiliwa kutokana na kazi nzuri iliyowaridhisha wengi, huku wengine ambao ni wapya na wana rekodi nzuri kwenye maeneo yaliyopo wakishangiliwa na wananchi kutoishiwa hamu ya kuwasikiliza.
Kwenye nafasi ya udiwani katika baadhi ya kata wamepaza sauti baadhi ya wagombea wao kukatwa wakati wao wanaona wanafaa, hali iliyilazimu CCM kubadili gia angani kwa kuwarejesha wagombea wote walioomba nafasi hizo, ili waende kwenye hatua ya kura za maoni kuomba ridhaa.
Hii ni ishara kuwa elimu ya uraia imewaingia wananchi wanaelewa wawahoji vipi wananchi wenzao wanaoomba nafasi za uongozi, wanakumbuka ahadi walizowapa, wanawafahamu vyema watu wanaogombea nafasi hizo kwenye maeneo yao.
Wananchi wanadhihirisha kuwa muda wa hukumu ni sasa, ni wakati wao wa kutamba, ingawa fitina zinaweza kupenyezwa kupunguza kasi baadhi ya wagombea.
Pia si kwamba wanachama wa CCM pekee ndio wana wajibu wa kuwahoji wanaogombea bali wananchi wote, ambao iwapo kiongozi huyo atapewa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama hicho, na kuingia kwenye kiny’ang’anyiro na kuibuka mshindi atawaongoza wote.
Jambo hili lina tafsiri nyingi, mosi ni mwamko mkubwa wa Watanzania kwamba wanataka viongozi wawajibikaji na si wale wanaoomba uongozi na kwenda kuishi mjini au nje ya majimbo husika, na kutoshughulika na matatizo ya wananchi au kupaza sauti katika mhimili wa Bunge.
Unapoomba udiwani, ubunge na uwakilishi ni kazi ya kuwatumikia wananchi, wao ndio waajiri wao, hivyo unawajibu wa kubeba dhamana kwa uzito mkubwa na kushiriki kwenye maendeleo yao, kwa kuwa wananchi wanamjua anayewapenda.
Sura nyingine ni kuwa hata mgombea akitoa rushwa bado wananchi watampima kwa mizani ya uwajibikaji, jambo ambalo ni zuri kwa kuwa litaongeza uwajibikaji kwa wanaoomba nafasi za uongozi.
Lakini wananchi wamepaza sauti pia, wakisema hawataki wabunge wasioweza kuwasemea bungeni,wakieleza matarajio yao kwa ambao watachaguliwa kwa nafasi mbalimbali.
Tunaamini kupitia mchakato huo, wagombea na wananchi wamejifunza mengi likiwamo kubwa la dhamana wanayoiomba kwa Watanzania, kwenda kuwajibika ipasavyo kuwasemea na kutatua kero zao kuanzia ngazi ya halmashauri hadi bungeni.
Ni fundisho kwa waliokuwa viongozi katika nafasi mbalimbali kwamba wanapaswa kuwajibika ipasavyo, kupima ahadi wanazotoa kwa wananchi kwamba zinatekelezeka, kwa kuwa baada ya miaka mitano zitakuwa kifungo kwao.
Ni muhimu vyama vingine vikafanya mchakato wa namna hiyo kwa wagombea kwenda kwa wananchi kujieleza, kisha waulizwe maswali, ili inapofika wakati wa kuanza kwa kampeni wananchi wasikilize sera zao kisha kufanya maamuzi sahihi kwenye sanduku la kundi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED