PAZIA la Uchaguzi Mkuu 2025 limefunguliwa rasmi kwa wagombea wa vyama vitatu kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kupeperusha bendera za vyama vyao Oktoba 29, mwaka huu kwa ajili ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Saba.
Uchukuaji fomu ulianza kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa na mgombea mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kuchukua fomu katika Ofisi za INEC eneo la Njedengwa, Dodoma.
Aidha, mgombea urais wa Chama cha National Reconstraction Alliance (NRA) Hassan Kisabya, akiwa ameambatana na mgombea mwenza, Hamisi Ally Hassan naye alifika INEC na kukabidhiwa fomu ya uteuzi.
Pia Chama Cha Wakulima (AAFP) Kunje Ngombale Mwiru akiwa na mgombea mwenza Chumu Juma Abdalah, walichukua fomu.
Wagombea hao ni kati ya wagombea urais wa vyama 18 vilivyosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi 2024 kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu.
Sasa ni rasmi kumekucha na kila chama kimeanza mbio za kusaka idhini ya Watanzania kuongoza Serikali ya Awamu ya Saba kupitia sanduku la kura zitakazopigwa Oktoba 29, mwaka huu.
Rais Samia anaandika historia ya kipekee Tanzania kwa kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza kushika madaraka baada ya Rais John Pombe Magufuli kufariki dunia, na kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Historia hiyo inajikita kwa kuwa mwanamke wa kwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho Januari mwaka huu, kupeperusha bendera ya chama hicho.
Sasa amechukua fomu akionesha utayari wake wa kuomba ridhaa kwenye jukwaa la kisiasa katika mikutano mbalimbali, kuongoza Serikali ya Awamu ya Saba, kwa ajili ya kukamilisha historia nyingine.
Kufunguliwa kwa pazia la kuchukua fomu ya uteuzi wa urais kwa siku sita kwa vyama 18 kuchukua fomu INEC kisha Tume kuanza vikao vya uteuzi ambavyo vitakamilika Agosti 27, mwaka huu.
Aidha, Agosti 28, mwaka huu ndio kampeni rasmi kwenye udiwani, ubunge na rais ziataanza kwa siku 60 kabla ya siku ya uamuzi mgumu Oktoba 29, kwenye sanduku la kura.
Hatua hii ni sawa na mashindano ya mpira kwamba kipenga kimepulizwa sasa wachezaji 18 wameingia uwanjani kila mmoja akiwa na mbwembwe zake za kuonesha anaweza kufunga goli zuri Oktoba 29.
Ni wajibu wa wapigakura kuwafuatilia kwa karibu wagombea wote ili kuwasikiliza tangu ulipoanza mchakato ndani ya vyama vyao na sasa wanakwenda INEC kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuongoza Tanzania.
Bila kuwafuatilia, kusikiliza sera zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi 2025-2030, mpigakura atafanya maamuzi ya kufuata mkumbo, hivyo ni muhimu kuwapima wagombea na vyama vyao kisha kufanya maamuzi ambayo hayatajutiwa miaka mitano ijayo.
Misingi thabiti ya Tanzania ilishajengwa na tayari kuna nyenzo muhimu kama Dira 2050 ambayo inaonesha mwelekeo wa Tanzania kwa kipindi chote, ikiwa na ulinzi thabiti wa kisheria ili kati ya wagombe 18 atakayeingia madarakani isiibadilishe na kupuyanga akatavyo.
Hivyo,tusimame kwenye nafasi yetu wapigakura kuamua nani kiongozi imara na thabiti wa kumwajiri kuongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo ili tusijesema tungelijua, wakati tumeshang’atwa na nge.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED